TESDO MAKAO MAKUU TABORA

tesdo makao makuu

Usajili utafanyika kwa vituo vitatu, TABORA,DODOMA na DAR ES SALAAM, unatakiwa kudownload fomu kwenye blog ya asasi na kuijaza vyema, kisha unatakiwa ulipie ada ya uanachama na fomu kama inavyojieleza kwenye hiyo fomu. Akaunti no 01522250952400. Kwa kituo cha TABORA utakabidhi fomu yakokwa Mohamed Mapalala 0715449745, DODOMA Zahoro HM na Malale Buluba 0764492146. DAR ES SALAAM Mayasa Mzelela 0785314908, kasha baada ya muda utapatiwa risiti yako. Fomu inapatikana sehemu ya TESDO DOCUMENTS. Kwa maoni kuhusu utaratibu tuma kwenye email tesdo@rocketmail.com au simu 0716555450/0785314908.

Hamisi Masoud Mtwale

Mwenyekiti TESDO



Monday, March 12, 2012

Tabora Marathon na changamoto za maboresho

MJI wa Tabora na vitongoji vyake, juzi Jumamosi ulikuwa kwenye hekaheka za mashindano mapya ya mbio yaliyopewa jina la Tabora Marathon 2012, yaliyohusisha wanariadha chipukizi yakiwa na nia ya kufufua vipaji vya mchezo huo kwa mkoa huo na ile ya jirani.
Zaidi ya wanariadha 200 walikuwa wakitimua vumbi kuwania zawadi mbalimbali, katika mbio za kilomita 21 zilizoanzia Orion Hotel, kupitia barabara za Boma, Swetu, Sikonge na kuishia viwanja vya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere, pamoja na zile za kujifurahisha za km tano zilizohusisha washiriki wa umri tofauti.
Katika mashindano hayo, Dikson Mkami, aliibuka mshindi kwa wanaume, kama ilivyokuwa kwa Rozy Seif, aliyeshinda kwa wanawake na kila mmoja kujinyakulia zawadi ya shilingi 100,000, huku washindi wa pili wa kila upande wakitoka na zawadi ya shilingi 80,000 na wa sh 50,000.
Baada ya kumalizika kwa mashindano hayo, waratibu kupokea ahadi kutoka serikali ya mkoa ya kuyafanyia maboresho msimu ujao, Mshauri wa Ufundi wa Tabora Marathon, Tullo Chambo, akabainisha mipango ya kina ya kufanya makubwa zaidi katika mbio hizo msimu huo.
Chambo katika mahojiano na gazeti hili, alisema washiriki walikuwa zaidi ya 200, lakini safari ijayo anatarajia washiriki watakaojitokeza wataweza kufikia zaidi ya 400, huku akisisitiza zawadi zitaboreshwa zaidi, ikiwamo washindi kupewa ofa ya kusomeshwa kozi mbalimbali chini ya udhamini wa makampuni yatakayosapoti mbio hizo.
“Nashukuru sana mbio hizi zimefana sana na hakuna mshiriki aliyepata, madhara ama kuumia, natarajia kufanya kitu kikubwa zaidi hapo mwakani na mipango hiyo inaazia rasmi sasa.” alisema Chambo.
Alisema amejifunza mengi sana katika mbio za Kilimanjaro Maratahon, hivyo anataka Tabora Marathon nayo iwe mfano wa kuigwa.
Aidha, Chambo anasema yeye ni mzaliwa wa Mkoa wa Tabora na pia amepata masomo ya awali katika Shule ya Msingi Kitete ambapo kipindi hicho alikuwa akipenda sana mchezo wa riadha na alikuwa akishika nafasi nzuri pale yanapokuwapo mashindano shuleni hapo.
Hata hivyo anapenda kutoa changamoto kwa uongozi wa riadha Mkoa wa Tabora, (RITAM) kuwa, mchezo wa riadha unahitaji maandalizi kama michezo mingine na kutoa wito kwa viongozi hao wajipange ili mashindano yajayo kuwe na mipango mizuri itakayovutia washiriki.
“Nina nia njema na Mkoa wa Tabora ambao kwa sasa kila mchezo umedorora. Lakini mimi ni mtaalamu wa mchezo wa riadha, hivyo sidhani kama nitashindwa kufanikiwa katika hili. Natoa wito kwa serikali, viongozi wa michezo na makampuni mbalimbali, hasa ya tumbaku kuwekeza kwenye riadha kwani utatoa ajira kwa vijana walio wengi,” alisema Chambo.
Katika mashindano ya mwaka huu, serikali imesifu ubunifu uliofanywa na Mshauri huyo wa Ufundi, sanjari na Mratibu wa mashindano hayo, Ramadhan Makula, kushirikisha vijana, wazee na watoto katika mbio hizo.
Hali hiyo imefanya hata serikali kuunga mkono ubunifu huo ambao pia umelenga kuutangaza Mkoa wa Tabora na vivutio vya utalii, hali ambayo itasaidia kupata watalii wa ndani na nje kupitia historia ya makumbusho na Kwihara.
Naye mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa, ambaye alizindua mbio hizo, alisema amefurahishwa sana na mpango huo ambao sehemu kubwa ni ajira.
Mwassa katika nasaha zake aliwashukuru wadhamni wakuu wa mashindano hayo, Kishen Enterprises Ltd, Azania Wheat Flower, NGS Investment CO LTD ya mkoani Shinyanga ambao ni wanunuzi wa pamba, Dash Communication wauzaji wa sabuni jijini Dar es Salaam kwa kuweza kufanikisha mashindano hayo.
Mkuu huyo wa mkoa aliwapongeza Mshauri wa Ufundi, Tullo Chambo, ambaye pia ni Mhariri wa Michezo wa gazeti hili na mratibu wa mashindano hayo, Ramadhan Makula, kwa kukubali kuwa na uzalendo na kuja nyumbani kuleta michezo licha ya wao kuwa nje ya mkoa kikazi.
Aidha, Mratibu wa mashindano hayo, Ramadhan Makula na Chambo, waliwashukuru washiriki wote waliojitokeza pamoja na kamati nzima ya mashindano hayo na kuomba radhi kwa kila mdau, endapo kulikuwa na upungufu na kueleza kuwa katika mashindano yajayo kasoro zote zitaondoshwa.
Habari na  Hastin Liumba
Makala Tanzania Daima

0 comments

Post a Comment